04:16
0
Dar es Salaam. Kocha Msaidizi wa Al Ahly, Ahmed Ayoub ameichambua Yanga kwa kusema ni timu bora katika kushambulia, lakini si nzuri kwenye safu ya ulinzi.

Yanga itaivaa Al -Ahly Jumamosi hii katika pambano la raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mahojiano na mtandao wa klabu hiyo, Ayoub alisema, ushindi wa jumla ya mabao 12-2 ilioupata Yanga dhidi ya Komorozine ni uthibitisho kwamba safu yake ya ushambuliaji ni moto wa kuotea mbali.

Katika michezo 17 ya Ligi Kuu Tanzania Bara safu ya ushambuliaji wa Yanga imefunga mabao 41 na kuruhusu mabao 12 hadi sasa.

“Yanga ina safu ya ushambuliaji yenye nguvu kwani imefunga mabao 12 katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa ilipocheza na Komorozine ambayo matokeo ya jumla ni 12-2,” alisema Ayoub.

Aliongeza: “Ina kikosi chenye nyota watano wa kulipwa kutoka Congo, Rwanda, Burundi na Uganda ambao wana mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji.”

Pamoja na kusifia safu ya ushambuliaji ya Yanga, kocha Ayoub alisema atatumia udhaifu wa ngome ya ulinzi kupata matokeo mazuri.

Alisema beki ya Yanga si imara kwani haina ushirikiano wa kutosha miongoni mwa wachezaji wake husika.

“Timu ya Tanzania ina udhaifu katika eneo la ulinzi ambako kimsingi hakuna muunganiko mzuri wa wachezaji wanaocheza eneo hilo,” alisema Ayoub.

Kocha huyo alishuhudia pambano la kwanza kati ya Yanga na Komoriozine lililopigwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Kauli ya kocha huyo ni changamoto kwa Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm kwani ni wazi anatakiwa kuisuka kikamilifu ngome yake ya ulinzi kabla ya mchezo kati yake na vigogo hao wa Misri.

Safu ya ulinzi ya Yanga inaundwa na mabeki wa kati Kelvin Yondani na Nadir Haroub pamoja na mabeki wa pembeni Oscar Joshua anayecheza kushoto na Mbuyu Twite kulia.

0 comments:

Chapisha Maoni

rightcolbanner