05:36
0
Ni wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea vyema na mishe mishe zako za kimaisha.

Mimi nimshukuru Mungu kwa yote mema ambayo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu ikiwa ni pamoja na kunipa nguvu ya kuweza kutimiza yale ninayostahili kuyafanya kwa jamii yangu.

Wiki hii msomaji wangu nataka kuzungumzia jinsi mke wa mtu au mwanamke mwenye mpenzi wake anavyoweza kuwakwepa wanaume wakware.

Nimekuwa nikipata malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wasomaji wangu wakielezea jinsi wanavyosumbuliwa na wanaume, wengine wakidai wanataka kuwaoa, wengine wakieleza wazi kuwa wanataka kufanya nao mapenzi tu tena kwa ahadi mbalimbali.

Kimsingi hili ni tatizo sugu ambalo linaepukika lakini kuna ugumu kidogo katika kuliepuka moja kwa moja. Mitaani tunakoishi wapo wanaume ambao wasione msichana mrembo akipita, lazima wataanza kumsumbua kwa kumuita na wengine kufikia hatua ya kuwafanyia vitendo vichafu. Mbaya zaidi ni kwamba wanaume hao hufanya hivyo hata kwa wanawake ambao ni wake za watu au wenye wapenzi wao.

Tabia hii huwakera sana baadhi ya wanawake hasa wale wanaojiheshimu na kuziheshimu ndoa na mahusiano yao.
Hata hivyo, kuwaepuka wanaume wakware wakati mwingine huwa ngumu kwa kuwa wengi wao ni micharuko, yaani hawajali wala kufikiria kinachoweza kuwapata baadae.

Niseme tu kwamba, wanaume wa aina hii wapo wengi tu huko mtaani ila kwa mwanamke anayeiheshimu ndoa yake au uhusiano wake na akaweka nia ya kuwaepuka, inawezekana! Nikupe tu baadhi ya mbinu ambazo zinaweza kukusaidia kuondokana na usumbufu kutoka kwa wanaume wakware.

Punguza ukaribu, acha utani na wanaume

Wanawake wengine ni wa ajabu sana. Unamkuta anajenga ukaribu sana na baadhi ya wanaume na kufikia hatua ya kutaniana nao katika mambo ambayo mwishowe huwa kutongozana.

Mwanamke aliyeolewa ama mwenye mpenzi wake hatakiwi kujenga ukaribu sana na wanaume wa pembeni. Cha msingi ni kuwaheshimu na kuwachukulia kama watu amambo akiwachekea anaweza kuja kuvuna mabua.

Unapopita sehemu ukakuta wavulana wamekaa, wasalimie kisha chukua hamsini zako, utani utani wa kijinga epukana nao kwani mwisho wa siku watakutongoza na ukionesha kuchukia watadai walikuwa wanakutania kumbe wako ‘sirias’.

Usijishebedue kwao
Baadhi ya wanawake hujitakia wenyewe usumbufu kwani tabia zao huwafanya wasiheshimike mbele ya jamii na kuonekana kwamba ni jalala. Unakuta mwanamke anapita mbele za wanaume kisha anatembea kwa kujishebedua huku akitingisha mauno yake makusudi, hapo unatarajia nini?

Achilia mbali hilo, wapo baadhi ya wanawake ambao ni rahisi kuchukuliwa na wanaume. Yaani hawawezi kusena hapana! Ukiwa na tabia hiyo tambua tu kwamba, kila mwanaume atakusumbua. Jiheshimu na wanaume nao watakuheshimu na hawatakuwa na muda wa kukutamkia maneno yasiyofaa.

Mavazi ya kimitego yapotezee
Wanawake wengi sana hukosea katika suala zima la uvaaji. Baadhi yao hupendelea kuvaa mavazi yanayoonesha maungo yao kiasi cha baadhi ya wanaume kuwachuklulia kuwa ni machangudoa.

Ni kweli kwamba mavazi ya mtu hayawezi kumfanya akaingizwa katika kundi la watu fulani na pia kila mtu anao uhuru wa kuchagua avaeje lakini, kwa uhalisia mwanamke asiyeujali mwili wake kwa kuvaa nguo zisizokuwa na heshima, asitarajie kuuepuka usumbufu wa wanaume wapenda ngono. Ni lazima watamtongoza na wakati mwingine kumfanyia vitendo vya kumdhalilisha.

Nadhani ifike wakati uondokane na ulimbukeni wa kwenda na wakati hasa kwa wewe mwanamke ambaye umeolewa ama una mpenzi wako. Vaa mavazi ya heshima kila unapokwenda.

Mavazi yanayoonesha mauno yako yavae ukiwa na mpenzi wako chumbani. Naamini kwa kuvaa hivyo, kidogo utakuwa unapunguza ile kasi ya wanaume wakware kukusumbua.

Niseme tu kwamba, wanaume siku hizi wametawaliwa na tamaa zisizokuwa na msingi. Ukitaka wakusumbue watakusumbua kweli na wakati mwingine wanaweza kukushawishi ukamsaliti mpenzio wako.

Kikubwa ni mwanamke kuwa na msimamo. Kutokukubali kugeuzwa kiti cha daladala kwamba kila mtu anaweza kumchezea. Naamini msimamo huo pamoja na mambo hayo niliyoyataja hapo juu unaweza kuepukana na usumbufu huo kutoka kwa wanaume wakware.

Usipokuwa makini na haya niliyoyazungumza leo, inamaanisha uko tayari kusumbuliwa na uko tayari kuachwa na mpenzi wako. Kuwa makini.

Niishie hapo kwa leo, tuonane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali.

0 comments:

Chapisha Maoni

rightcolbanner