08:34
0
Kumekuwa na vyama vingi vya wafanyakazi, lakini kero za wafanyakazi bado zinaendelea kuwapo.

Kwa mfano kuna vyama vya wafanyakazi vyenye lengo la kutetea walimu, hata hivyo bado walimu wengi wanaendelea kuteseka.

Hivi karibuni nilikuwa nazungumza na mwalimu mmoja, anasema anashindwa kuelewa maana hasa ya kuwapo kwa vyama vya wafanyakazi.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mwalimu wa Shule ya Sekondari Mbalizi ambaye hakutaka kutajwa jina lake huku akifafanua kwamba kama kweli Chama cha Wafanyakazi (CWT) ingekuwa ni kwa ajili ya wafanyakazi ingefungua kesi kudai madeni ya walimu.

Mwalimu huyo anasema pamoja na kwamba CWT inaongoza kwa kukusanya fedha za wanachama wake, walimu wanaongoza kwa kukopa na kuishi kwenye mazingira magumu zaidi nchini.

Imefikia hatua baadhi ya wafanyakazi wanaona kama vyama vya wafanyakazi vipo kwa ajili ya matumbo yao.

Mfanyakazi wa kampuni ya usafirishaji, Juma Hamisi anasema pamoja na kuwapo kwa chama chao cha Cotwu, lakini waajiri wanawakandamiza wafanyakazi.

Anasema madereva wamekuwa wakipewa Sh20,000 za posho ya safari ya kwenda kulala nje ya kituo cha kazi, je hiyo ni haki?

Pamoja na hoja hizo, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu, Utafiti na Kazi zinginezo (Raawu), Kanda ya Nyanda za Juu, Joseph Sayo anasema wafanyakazi wengi wamefaidi matunda ya kazi za vyama vya wafanyakazi.

Anataja moja ya faida kuwa ni Serikali kuondoa kodi kwa mishahara ya kima cha chini na pia kupunguza walau asilimia moja ya kodi kwa mishahara mingine yote.

Hata hivyo, anasema pamoja na faida hizo ukweli ni kwamba wafanyakazi wengi hawajajiunga kwenye vyama vya wafanyakazi.

Anasema vyama vya wafanyakazi vimefanya mambo mengi mazuri, yakiwamo ya kutetea sheria za kazi zirekebishwe na pia vyama vinasaidia kuendesha kesi nyingi za wafanyakazi.

0 comments:

Chapisha Maoni

rightcolbanner