KWAKO Msanii wa filamu Bongo, Yobnesh Yusuph ‘Batuli’. Pole na mihangaiko ya kujitafutia mkate wa kila siku. Naamini mishemishe zako zipo poa. Kwa upande wangu mimi naendelea vizuri. Naamini sijawahi kukuandikia barua hata mara moja, lakini nimeona ni vyema tuwasiliane kwa njia hii.
Lengo la kukuandikia barua hii ni kwa ajili ya kukuweka sawa, maana naona kama njia unayoanza kupita siyo! Wenyewe wamekataza! Kwa muda mrefu nimekuwa nikivutika na uigizaji wako, kama mdau wa sinema nchini nilikuweka miongoni mwa wasanii wenye uwezo mkubwa sana wawapo nyuma ya kamera.
Niliishia kuamini kuwa wewe ni msanii mkali, ambaye pengine siku zijazo utakuwa nyota. Ni kweli, kwa sasa katika wasanii walio kwenye nafasi za juu kabisa kwenye soko la filamu Bongo ni pamoja na wewe.
Najua jambo hili wengine hawapendi kukubaliana nalo hasa wasanii wenzako, lakini nataka kukuhakikishia kuwa uko matawi ya juu kabisa.
Najua jambo hili wengine hawapendi kukubaliana nalo hasa wasanii wenzako, lakini nataka kukuhakikishia kuwa uko matawi ya juu kabisa.
Wakati fulani nilipata kufanya mahojiano na wewe nikiwa na jopo la wahariri wenzangu. Hapo ndipo nilipogundua kuwa kumbe una uwezo mwingine zaidi ya sanaa. Niligundua kuwa una uwezo mkubwa wa kufikiri tofauti na matarajio ya wengi.
Kusema kwamba, ulitakiwa kucheza Filamu ya O’prah katika nafasi iliyochukuliwa na msanii mwingine ili ushiriki kwenye vipande vya kimahaba (love scenes) – ukakataa kilidhihirisha ukomavu wa uelewa kichwani mwako!
Nilikusifu kwa hilo. Mpaka sasa naendelea kukusifia kwa hilo. Naamini hata mashabiki wako wanakusifia kwa hilo maana ni jambo kubwa na la maana sana.
Nikiwa nimekuweka kwenye nafasi hiyo, wiki iliyopita nikashangazwa na jambo lililotokea kuhusu wewe. Nikajiuliza: Hivi ni Batuli huyuhuyu ninayemjua au mwingine?
Batuli aliyekataa kucheza sinema yenye maudhui ya kimapenzi kwa hofu ya kuharibu jina lake, leo hii anaweza kusema yupo tayari kucheza sinema za aina hiyohiyo lakini nje ya nchi? Nikapigwa na butwaa. Batuli amechanganyikiwa? Nikawaza.
Naamini hata kama ungekuwa ni wewe ungechanganyikiwa kama mimi. Batuli, kwani hiyo sinema ukienda kucheza Nigeria na kuvaa mavazi ya hovyo, haitasambazwa hapa Bongo na hatimaye wadau wakaiona?
Umesema tamaduni za nchi nyingine ni tofauti na zetu, ndiyo maana unaweza kwenda kucheza, sawa lakini vipi kuhusu maadili yako kama Mtanzania? Ukionekana kwenye sinema hata kama ni ya Marekani, umevaa vivazi vya ajabu, itabadilisha jina lako la Yobnesh?
Sinema chafu hata ukicheza wapi, bado haiwezi kukubadilisha Batuli, haiwezi kukuondolea Utanzania wako. Haiwezi kubadili chochote. Kila kitu kitabaki katika uhalisi wake uleule!
Nadhani hukufikiri vizuri na kama mtazamo wako bado ni huo, nakuomba sana tafakari tena – hauko sahihi. Jamii inakuamini sana, una uwezo mkubwa wa kuwa staa zaidi ya ulivyo huku ukiendelea kuhifadhi maadili yetu.
0 comments:
Chapisha Maoni