22:36
0

NAJUA nitawakera wengi sana kwa kuandika habari zinazomhusu Wema Sepetu, msichana mwenye jina kubwa Bongo, lisilofanana na kazi anayoifanya, kwa sababu wapo wanaompenda sana na wengine wamechoshwa naye.
Lakini kama kaka, ninalazimika kuandika kwa mara nyingine kuhusiana na mambo yake, baada ya kuwa nilishawahi kufanya hivyo siku za nyuma, lengo langu kubwa ikiwa ni kumpa ushauri wa bure, ambao kama ataupokea na kuufanyia kazi, unaweza kumsaidia, angalau kwa mambo ‘madogo madogo’.
Jumatatu wiki hii, Wema alifanya kituko cha mwaka, tena safari hii, akizifuata kamera yeye mwenyewe, bila shaka baada ya kuona picha zake nyingi tulizonazo hazitoshi. Akiwa na hasira, msichana huyo aliibuka chumba chetu cha habari kama utani vile.
Walinzi walimruhusu kuingia katika lango kuu akiambatana na wapambe wake wachache dhaifu kwa vile waliamini kuwa alishafanya mawasiliano na mmoja wa waandishi wetu kama inavyotokea mara nyingi. Lakini ghafla akiwa ndani, akageuka mbogo, akitukana matusi mazito ya nguoni huku alioandamana nao wakifanya.
Waandishi wetu na walinzi walijaribu kumsihi atulize mzuka, lakini hakusikia. Hata hivyo, waliendelea kuwa watulivu hadi askari Polisi walipofika. Kwa kuamini kuwa ana matatizo ndani ya kichwa chake, uongozi uliwashauri askari hao kuondoka bila kumchukua, kwani tayari hali ilishadhibitiwa.
Tukio hilo limemalizika kimya kimya kwa sababu kampuni inaamini kwa kumfungulia mashtaka, ya kufanya fujo ofisini na kutukana matuzi mazito, itakuwa ni kumuongezea matatizo badala ya kumsaidia, kwani kwa kiasi kikubwa, Wema anahitaji msaada wa kisaikolojia, ili akili yake ikae katika mstari ulionyooka.
Huenda anaamini tayari yeye ni supastaa na sugu wa kesi, kwa vile aliwahi kupata vikesi kama viwili vitatu na kushinda mahakamani. Kesi ya kwanza ni ile ya kuvunja kioo cha gari la marehemu Steven Kanumba na nyingine ni ya kumpiga meneja wa hoteli moja iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam ambaye alijaribu kumtuliza wakati akileta fujo eneo hilo, bila shaka baada ya kulewa.
Siamini kama hizi ni kesi ‘siriaz’ ambazo mtu anaweza kujisifu kwa kushinda, kiasi cha kumfanya kuwa kiburi wa kuamini anaweza kufanya chochote mahali popote.
Wema Sepetu ni mmoja kati ya watu wenye bahati kubwa, ambao wanapaswa kumshukuru Mungu badala ya kumkufuru, kwanza kwa kumpa umaarufu mkubwa asiostahili na tena kwa kumnusuru na majanga mbalimbali kama hayo ya kunusurika kwenda jela.
Katika hali ya kulewa au kupenda sifa kupitiliza, kuna wakati aliwahi kutembea uchi jukwaani, hali iliyomfanya yeye na shoga yake, Aunt Ezekiel kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuomba radhi kwa tukio lile.
Katika umri wake mdogo, ana msururu wa wanaume wanaofahamika waliowahi kutoka naye kimapenzi. Nafikiri umefika wakati, mashabiki wake kufanya sala maalum ya kumuombea. Huenda kuna vitu vinamsumbua kichwani mwake kwa sababu baadhi ya matukio anayofanya, hayawezi kufanywa na mtu mwenye akili ya kawaida tu.
Nimsihi kwa mara nyingine Wema, atulize akili yake. Kama anadhani anaandikwa vibaya, hii yote ni kwa sababu yake mwenyewe. Watu wanamfuatilia kwa sababu alipotwaa Umiss Tanzania mwaka 2006, alijitengenezea sifa ya kuwa Public Figure. Na sifa hiyo akaamua kuitumia vibaya. Mbona kuna mamiss kibao wamepita baada au kabla yake lakini hawang’ai magazetini?
Asijiamini sana kwa sababu hana umaarufu wa kuishinda sheria na wala hana mkwanja wa kumzuia mtu ‘mwenye nazo’ aliyepania kumtupa jela. Katika nchi ambayo vyombo vyake vya dola na sheria vimeoza kwa rushwa kama yetu, zoezi la kumpoteza kwa upuuzi anaoufanya wala halihitaji ujuzi.
Ni vizuri akili yake ikakomaa kama mwili wake unavyokomaa, makosa ya jana yampe somo ili aweze kuchukua tahadhari na kujifunza kwa sababu maisha ya Uwema Sepetu yana mwisho.

0 comments:

Chapisha Maoni

rightcolbanner