Wanaume wawili wa nchini Iran wamehukumiwa adhabu ya kifo kwa kutengeneza na kuendesha tovuti ya picha na video za ngono. Mahakama za nchini Iran zimewahukumu watu wawili adhabu ya kifo kwa kuendesha tovuti ya ngono, shirika la habari la Iran, IRNA limeripoti.
"Watu wawili waliokuwa wakisimamia tovuti mbili tofauti za ngono wamehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama mbili tofauti, hukumu zao zimetumwa mahakama kuu ili zithibitishwe kabla ya kutekelezwa", lilisema shirika hilo la habari bila ya kutaja majina ya watu hao.
Mwezi disemba mwaka jana, serikali ya Canada ilielezea kusikitishwa kwake na raia wa Canada mwenye asili ya Iran kuhukumiwa kunyongwa kwa kutengeneza tovuti ya ngono.
Raia huyo wa Canada, Saeed Malekpour, 35, alipatikana na hatia ya kutengeneza na kuisimamia tovuti ya ngono ambalo ni kosa la kwenda kinyume na maadili ya kiislamu.
Malekpour alitiwa mbaroni nchini Iran mwaka 2012 baada ya kurudi nchini humo akitokea Canada ili kumuuguza baba yake ambaye alikuwa mgonjwa.
Alihukumiwa adhabu ya kifo mwezi disemba mwaka jana.
0 comments:
Chapisha Maoni