00:28
0
ZIKIWA zimesalia saa chache kabla ya mechi dhidi ya Al Ahly ya Misri itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, wabunge na mawaziri kadhaa walilazimika kufika kwenye kambi ya Yanga iliyopo Kunduchi katika Hoteli ya Ledger kwa ajili ya kuhamasisha.
Timu hizo zinatarajiwa kukutana katika mchezo huo wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Al Ahly ndiyo mabingwa watetezi wa ligi hiyo, lakini Yanga wamesema kuwa ushindi kwao ni lazima.
Morali hiyo ya ushindi imeongezwa na Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ambaye amesema anajua mbinu nyingi za Warabu hao na kusisitiza lazima Yanga ishinde na lazima ianze kufunga bao katika mechi hiyo.

Wabunge & mawaziri
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kambi hiyo zinaeleza kuwa ugeni huo ulifika kambini hapo juzi kwa nia ya kuwaongezea morali wachezaji na benchi la ufundi ili kuhakikisha ushindi unapatikana.
“Ugeni huo uliokuwa na zaidi ya watu 20, ulipokelewa na Seif Magari, ambapo umeahidi vitu vingi mbali na ile milioni mia moja iliyoandikwa kwenye magazeti. Nia ni kuhakikisha Al Ahly wanafungika,” alisema mtoa taarifa.
Pluijm ‘full’ tambo
Pluijm, raia wa Uholanzi, aliliambia gazeti hili katika mazoezi ya timu hiyo juzi kuwa Warabu hao wanapokuwa ugenini wanapenda kupoozesha mchezo bila sababu za msingi, lakini akasisitiza kuwa wamejipanga.
“Nawajua hawatanisumbua, nitahakikisha tunapata bao la mapema ili wasipate nafasi ya kuleta mpira wao wa kupoozesha mchezo.
“Tutapambana kuhakikisha hawapati bao hata moja ili tuwe na wastani na faida nzuri tutakapokwenda ugenini,” alisema Pluijm.

Mbinu mpya Yanga
Katika kuelekea mchezo huo kocha huyo alifanya mabadiliko kadhaa katika mazoezi yaliyofanyika juzi kwenye uwanja wa Boko Veterani uliopo nje kidogo ya Dar.
Kiungo Athumani Idd ‘Chuji’ alicheza nafasi ya beki wa kulia huku mshambuliaji Mrisho Ngassa akicheza nafasi ya kiungo mchezeshaji.
“Sijawabadili namba, nitaendelea kuwatumia kwenye nafasi zao zilezile, nilichokifanya hapa ni moja ya programu zangu zitakazosaidia baadhi ya vitu.
“Hata hivyo wamecheza vizuri, wameonyesha kumudu hizo nafasi,” alisema Pluijm.

Kikosi chatabiriwa
Kutokana na mwenendo wa timu hiyo katika mechi za hivi karibuni, kuna uwezekano mkubwa wa kikosi kitakachoanza kesho kuwa hivi:
1. Deo Munishi ‘Dida’, 2. Mbuyu Twite, 3. Oscar Joshua, 4. Kelvin Yondani 5. Nadir Haroub ‘Cannavaro’, 6. Frank Domayo, 7. Simon Msuva 8. Haruna Niyonzima 9. Didier Kavumbagu, 10. Emmanuel Okwi 11. Mrisho Ngassa

Ngassa anaongoza kwa mabao Afrika
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo amefunga mabao sita.

Yanga ipo kwenye ‘form’
Yanga imekuwa ikionyesha iwezo mkubwa katika mechi za hivi karibuni, ambapo iliifunga Komorozine ya Comoro jumla ya mabao 12-2 katika mechi mbili za raundi ya awali.
Baada ya hapo ikaitandika Ruvu Shooting mabao 7-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara, hivyo licha ya kuwa Al Ahly ni timu ngumu, rekodi hiyo inaweza kuwa chachu ya wachezaji wa Yanga kufanya vizuri.

Tambwe aiombea Yanga
Straika wa Simba, Amissi Tambwe amesema anaiombea Yanga  ipate ushindi katika mechi hiyo ya kesho.
“Yanga hawatakiwi kuogopa, wajiamini kuwa wanaweza, mpira umebadilika sana lolote linaweza kutokea lakini naiombea ishinde hapa nyumbani,” alisema Tambwe.  
 Upande wa Al Ahly walikuwa wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) ya Upanda, juzi na jana huku ulinzi ukiwa mkali ambapo, hakuna mwandishi aliyeruhusiwa kuingia au kushuhudia mazoezi hayo, lakini kwa kutumia ujanja, Championi Ijumaa lilishuhudia mazoezi hayo kupitia sehemu moja pembeni ya uwanja huo.

0 comments:

Chapisha Maoni

rightcolbanner