Akitangaza uamuzi wa kuachana na chama hicho juzi, Naibu Katibu Mkuu NLD Zanzibar, Khamis Haji Mussa alisema ameshindwa kuvumilia kitendo hicho alichodai kinadhalilisha chama.
“Kwa hiari yangu nimeamua kujiuzulu uanachama na kuacha wadhifa niliokuwa nao ndani ya NLD, jina zuri la tawi la Ustawi wa Kitaifa wa Demokrasia ni nadharia tu, vitendo vyake ni udikteta na ubabe... nashauriana na wanasheria kuona kama kuna kesi ya kufunguliwa,” alisema Mussa.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya NLD Zanzibar pia kutoa tamko la kumtaka Rais Jakaya Kikwete kufuta uteuzi huo, kwa madai walioteuliwa kutoka chama hicho ni mtu na mkewe hivyo kukosa sura ya Muungano.
Mussa alisema ameshindwa kuvumilia kwa sababu kitendo hicho kinadhalilisha chama na kinaashiria ukosefu wa misingi ya uwazi na uadilifu.
Alisema amefikia uamuzi huo kutokana na madai kwamba Dk Makaidi ameonyesha waziwazi anaiongoza NLD kwa ubinafsi, ubaguzi na kuitenga Zanzibar katika uwakilishi wa Bunge la Katiba. Mussa alisema Dk Makaidi amejidhihirisha ni mbaguzi na anaweza kuligawa taifa kwa misingi ya Uzanzibari na Utanganyika, ikiwa siku moja atabahatika kupewa dhamana.
Alisema utetezi uliotolewa na Dk Makaidi umekosa nguvu ya hoja, zaidi ametumia umwamba unaoweza kuvipaka matope vyama vingine vya siasa.
Katika utetezi wake, Dk Makaidi alisema NLD Zanzibar walichelewa kupeleka majina kwa Rais wa Zanziba na kwamba, kuteuliwa kwa mkewe hakuna matatizo kwa sababu ana sifa zinazotakiwa.
0 comments:
Chapisha Maoni