03:56
0
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema atagombea uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu anaamini kuwa ana sifa za kutosha.

Hii ni mara ya kwanza kwa Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa kuweka wazi uamuzi wake huo. Mwingine anayetajwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.

Sifa za mtu anayepaswa kuongoza Bunge hilo ni kuwa na shahada ya sheria kutoka katika chuo kinachotambulika pia kuwa na uzoefu wa kuendesha mijadala kama ya Bunge.

Akizungumza na gazeti hili jana, Sitta alisema pamoja na propaganda chafu zinazoenezwa dhidi yake, hatakata tamaa na kwamba ataendelea na msimamo wake huo ili nchi ipate Katiba bora.

“Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imeainisha sifa za mtu anayetakiwa kuwa mwenyekiti na mimi nina sifa na nina mipango mizuri ya kuwafanya Watanzania wapate Katiba bora kama ndoto ya Rais wetu (Jakaya Kikwete) ilivyo,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu njama za kumzuia asigombee nafasi hiyo, Sitta alisema “Haishangazi watu hao kutumia mbinu chafu… Hawana maadili, ndiyo maana wananihofia lakini sishtuki hata kidogo.”

Sitta ambaye pia ni mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), alisema wabaya wake wamekuwa wakieneza maneno ya uongo kwamba ikiwa atakalia kiti hicho, atasimamia mpango wa Serikali tatu.

“Wanasema Sitta ataruhusu Serikali tatu, sasa nashangaa maana wajumbe ndiyo wenye mamlaka hayo… wanaeneza propaganda kuwa nina mkataba na wapinzani ndiyo maana wananiunga mkono. Wanasema mambo ya ovyo kabisa,” alisema.

Sitta alisema wapinzani kama walivyo wajumbe wengine kutoka CCM na makundi mengine, wanamuunga mkono kwa kuwa wanaamini akikalia kiti hicho ataendesha Bunge hilo kwa misingi ya uwazi na haki.

“Mimi sina mkataba na wapinzani ila wao kama watu wengine wananiunga mkono kwa sababu wanajua nitatenda haki, nina rekodi nzuri katika kuliendesha Bunge la Tisa wala hiyo haina mashaka,” alisisitiza Sitta.

0 comments:

Chapisha Maoni

rightcolbanner