08:00
0

Takriban katika maisha ya wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao hupitia katika vipindi tofauti. Kama ulivyo umri wa Binadamu, ndoa hupitia katika kipindi cha utoto, ujana na uzee, na kila kipindi kina mambo yake na taratibu zake kama tulivyoona katika makala zilizopita ambazo kama wanandoa watashindwa kuzifuata basi huenda ndoa hiyo ikakumbwa na mtihani mkubwa, nao ni mtihani wa kuchokana.
Hivyo basi, sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa kunasababishwa na mwanamke, pale ambapo atashindwa kutumia nafasi yake na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa yao.
Leo InshaAllaah tutahitimisha mfululizo wa makala haya kwa kugusia baadhi ya nukta ambazo ni muhimu kwa wanandoa kuzizingatia kabla na hata baada ya ndoa yao.

DINI
Kigezo Kikuu cha kusimamisha ndoa ni Dini, na ndoa yoyote inapokuwa haikuzingatia kigezo hiki basi ndoa hiyo inakuwa ina misukosuko isiyoisha, na si tu  inapelekea wanandoa kuchokana, bali inapelekea wanandoa kutengana na kuchukiana. katika zama tulizonazo zama ambazo umagharibi umetawala katika mila na desturi zetu, kigezo cha Dini kimepuuzwa na familia nyingi za Kiislamu, na hata ainisho la  neno ‘Dini’ limefahamika vibaya; Dini inaonekana ni imani ya kuzaliwa nayo, na si matendo na utaratibu wa maisha ya mtu. Na hii kupelekea mafunzo mengi ya Mtume (Swalla Allaahu   ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutofahamika katika usahihi wake, kwa mfano ile Hadiyth mashuhuri ya Mtume (Swalla Allaahu  ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokewa na Imaam Al-Bukhaariy inayohimiza kumchagua mchumba mwenye Dini:

    (...فاظفر بذات الدين تربت يداك...)   

(mchague mwenye dini utafanikiwa), mafundisho haya ya Mtume (Swalla Allaahu  ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yamekuwa yanatafsiriwa vibaya na wakati mwingine hata na Mashaykh, kuwa mwenye Dini ni yule Muislamu, hata kama haivai hijaab,  haswali, fedhuli, lakini muda wa kuwa amezaliwa Muislamu basi huyo ana Dini, ufahamu huu umewaingiza wanandoa wengi katika mitihani.

Bali wakati mwingine, unamkuta msichana amejihifadhi vizuri, anaswali lakini akhlaaq zake mbaya, msengenyaji, mfitinishi, hapendi ndugu wa mume, mchoyo na imani ya kweli haijagusa katika moyo wake, yeye huvaa Hijaab kama sehemu ya mila, na anaswali Swalah tano kutokakana na makuzi yake na mashinikizo ya kijamii, lakini hamna athari yoyote inayopatikana.

Hivyo basi, ni muhimu kwa wanandoa wahakikishe kuwa ndoa yao inajengwa katika msingi mkuu na imara, msingi wa Dini kwa maana yake sahihi.

 HALI YA KIJAMII NA KIUCHUMI
Katika ujenzi wa ndoa imara, kuna vigezo vingine ambavyo si muhimu lakini  havipaswi kupuuzwa, miongoni mwa vigezo hivyo ni kiwango cha wanandoa kijamii na kiuchumi, hiki ni kigezo ambacho kinaweza kuonekana ni cha kidunia zaidi, lakini uzoefu unaonyesha kuwa kimekuwa ni moja miongoni mwa sababu zinazopelekea chokochoko katika familia na hatimae kuikwaza ndoa yenyewe.

Inapotokea kwa mmoja miongoni mwa wanandoa hususan mwamume akawa na hali duni kiuchumi kuliko ile ya mkewe (familia ya mkewe) basi pamoja na mapenzi yanayowaunganisha, maisha yao yatakuwa na tahadhari kubwa sana, na wakati wowote kinaweza kutokea kitu ambacho hakikutarajiwa na kikazua mtafuruku.

Hivyo basi, ni vema wanandoa wakaanza kujenga misingi imara ya ndoa yao kwa kujitahidi kuzingatia kigezo hiki cha Kiuchumi na Kijamii.
 
KIWANGO CHA ELIMU
Aidha ni muhimu kigezo hiki nacho kikazingatiwa katika ujenzi wa ndoa imara, kwani wanandoa kama tulivyoona katika makala zilizotangulia, wanahitaji kuwa na mazungumzo baina yao, mijadala tofauti tofauti na kubadilishana mawazo katika maisha, inapokuwa elimu ya mwanamke ni kubwa kuliko ya mwanamume, kwa mfano, mwanamke anapokuwa na shahada ya Chuo Kikuu, na mwanaume ya Darasa la Saba, hapa panahitaji hekima na juhudi kubwa kwa mwanamke kuweza kumuelimisha mumewe bila ya kumfanya ajihisi mjinga, zoezi ambalo ni gumu, na uwezekano wa kushindwa ni mkubwa. Mwandishi wa makala hii, ana ushahidi tosha wa ndoa zilizoharibika kutokana na kigezo hiki. Nawe msomaji unaweza kufanya utafiti wako binafsi kuhusu hoja hii.
 
KABILA
Uislamu unayazingatia makabila kuwa ni sehemu ya watu kufahamiana, na si vinginevyo, na umekaripia vikali ubaguzi wa aina zote zile ukiwemo ubaguzi kwa misingi ya ukabila, utaifa, na rangi, na katika hili kuna Aayah nyingi sana na Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu  alayhi wa aalihi wa sallam).

Kwa upande mwingine, jamii zetu za Kiislamu bado kwa kiwango kikubwa zinajenga mahusiano katika misingi ya ukaribu wa kikabila na uzoefu wa pamoja, Uislamu haujakataza mtu kujinasibisha na nasaba yake, kuipenda na kuitakia kheri, bali uislamu umekataza mtu kujifakharisha kwa ukabila na kudharau makabila mengine.
Jamii za Kiislamu pamoja na kuunganishwa na Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini pia kila jamii inaunganishwa na vionjo vyake, na urfu zake ambazo huenda zikawa tofauti na jamii nyingine ya Kiislamu. Kwa mintarafu hiyo, ndoa inayowajumuisha watu wa kabila moja, inakuwa ina uimara zaidi kuliko ndoa tofauti, na inakuwa haina mashinikizo hasi kutoka katika jamii ukilinganisha na ile nyingine.

 NDUGU WA KARIBU
Uislamu umeruhusu kwa baadhi ya ndugu wa karibu kuoana, mfano mtoto wa baba mkubwa kwa baba mdogo, mama mkubwa kwa mama mdogo, mjomba kwa shangazi, na ndoa hizi zimeenea sana katika baadhi ya jamii, na hata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuozesha binti yake Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha)  kwa mtoto wa ammy yake ambae ni 'Aliy Bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu), jambo la kushangaza ni kuwa baadhi ya Waislamu hususan huku Afrika wamejiharamishia ndoa za aina hiyo, bila ya dalili, jambo ambalo ni kwenda kinyume kabisa na mafundisho ya Kiislamu.
Ndoa za ndugu wa karibu, zinaweza zikawa ni sababu ya kuimarika kwa ndoa au sababu ya kudhoofika, lakini kwa uzoefu wetu imeonekana kuwa ndoa za aina hii mara nyingi zinafikia katika hatua ya uzee mapema zaidi, hii ni kutokana na kufahamiana kwa ndugu hawa tangu utotoni, na kila mwanandoa kutotarajia jipya kutoka kwa mwenzake.

HITIMISHO
Ndoa ndio msingi wa Familia, na familia ndio tofali la kwanza la kujenga Jamii na hatimae kujenga Ummah, ndoa ni hatua muhimu sana anayopitia bianadamu katika maisha yake, na ndio hatua inayoiathiri maisha ya mtu na maisha ya kizazi chake baadae. Ni muhimu mtu kuwa makini sana na hatua hii.
Kwa wale ambao tayari wameishaingia katika hatua hii, basi ni muhimu kwao kuizatiti ndoa yao na mafundisho sahihi ya Uislamu na kujaribu kurekebisha madhaifu yao kwa kuwa wawazi baina yao na kupeana mawaidha kwa njia ya upole na hekima.
Maradhi ya kuchokana katika maisha ya ndoa ni maradhi yalioenea kwa wanandoa wengi, wapo wengine ambao hudhihirisha wazi hisia zao hizo kwa wenziwao, na wengine ambao huwa wanajaribu kuficha hisia hizo.
Ni jukumu la kila mwanandoa kuelewa ukweli huo, na kujaribu mara kwa mara kuleta mabadiliko mema katika maisha yao, au kuikarabati ndoa kwa maana nyepesi.

0 comments:

Chapisha Maoni

rightcolbanner